Header

Jonas Mkude atibuana na wachezaji wenzake wa Simba

Kikosi cha Simba, leo hii kikitarajia kuingia kambini kujiandaa na mechi yake ya Jumamosi dhidi ya Prisons ya jijini Mbeya, balaa jipya limeibuka ndani ya kikosi hicho linalomhusu nahodha wa timu hiyo, Jonas Mkude.
Baadhi ya wachezaji wa timu hiyo wanadaiwa kumtaka kocha mkuu wa timu hiyo, Mcameroon, Joseph Omog kumpokonya Mkude cheo cha unahodha wa klabu hiyo kutokana na vitendo vyake vya utovu wa nidhamu ambavyo amekuwa akifanya kila wakati klabuni hapo.
Wachezaji hao wamefikia hatua hiyo baada ya kutofurahishwa na kitendo cha Mkude cha kutojiunga na timu hiyo katika safari ya kwenda mkoani Ruvuma kwa ajili ya mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Majimaji pasipo kuwa na sababu zozote za msingi.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya Simba ambazo Championi Jumatano limezipata zimedai kuwa kutokana na hali hiyo Omog amewataka wachezaji hao kutulia na kuwahakikishia kuwa atalifanyia kazi suala lao hilo na kwa kuanza kumpa nafasi ya kucheza dhidi ya Prisons siku ya Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
“Wachezaji wengi hawafurahii kabisa tabia ya Mkude kwani hata leo hii (jana) katika mazoezi yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Chuo Kikuu cha Polisi, Kurasini ameelezwa.
Wamemwambia kuwa hawafurahii kuendelea kuongozwa na nahodha ambaye ndiye kinara wa utovu wa nidhamu ambaye amekuwa hana uchungu na timu na wakamkumbishia matukio yote kama hilo kukacha kwenda Songea pasipo sababu yoyote ya msingi lakini pia alifanya hivyo wakati tulipokuwa tunakwenda Zanzibar katika michuano ya Kombe la Mapinduzi.
Hakuambatana na timu na kuja siku iliyofuatia peke yake jambo ambalo lilimfanya kocha ampige benchi katika mechi ya kwanza ya michuano hiyo,” kilisema chanzo hicho cha habari.
Alipotafutwa Omog ili aweze kulizungumzia suala hilo hakupatikana kutokana na simu yake ya mkononi kuita bila ya kupokelewa.
SOURCE: CHAMPIONI

Comments

comments

You may also like ...