Header

Vita ya TRA vs TFF juu ya ukwepaji kodi yafikia hapa

Ni mwezi mmoja sasa umepita tangu Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ifunge Ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutokana na deni la kodi la muda mrefu vita hiyo sasa inakaribia ukingoni.

TRA imesema mambo yao na TFF yanaendelea vizuri na huenda yakakamilika wakati wowote kwa kuwekeana utaratibu mpya wa kulipana deni hilo.
Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo amesema “Tumefikia pazuri katika mazungumzo na TFF ili wamalize deni lao, tunaelekea kuweka utaratibu mzuri wa wao kutulipa.”
TRA ilifunga ofisi hizo tangu Machi 15, mwaka huu kutokana na deni kubwa la muda walilokuwa wakidaiwa TFF kupitia Kampuni ya Udalali na Minada ya Yono, ambayo kwa sasa ndiyo inazishikilia ofisi hizo baada ya kuwatoa nje wafanyakazi wote wa TFF na kuwataka waache kila kitu ndani.
Deni hilo ambalo zaidi linatokana na kodi ya mishahara ya aliyekuwa Kocha wa Taifa Stars, Mbrazili, Marcio Maximo kwa miaka minne kuanzia mwaka 2010 hadi 2016 huku deni lingine linalosababishwa ofisi hizo kufungwa ni la Kodi ya Ongezeko la Thamani (VaT)  ya mechi ya Taifa Stars na Brazil mwaka 2010.
Mapema wiki hii, Yono ilikamata basi la TFF lililopaswa kuibeba timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17 (U-17), Serengeti Boys iliyokuwa ikienda kupata chakula cha jioni na Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu. Hata hivyo, basi hilo liliachiwa baadaye.
Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas alipotafutwa alisema: “Suala la TRA limechukuliwa na Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo ambapo waziri wake, Dk. Harrison Mwakyembe amemuagiza katibu wake amtafute katibu wa hazina halafu baadaye tukutane wote kwa pamoja kulijadili na nikiongea nje ya hapo nitakuwa nakosea.”
SOURCE:Gazeti La Championi

Comments

comments

You may also like ...