Header

Diamond kuja na album ya Bongo Flava tu, afafanua uandishi wa nyimbo zake za kimataifa

Diamond Platnumz ametolea ufafanuzi mtindo wake wake wa uandishi katika nyimbo anazozilenga kuvuka nje ya Tanzania. Amesema kuwa, nyimbo za aina hiyo zikiwemo Marry You aliyomshirikisha Ne-Yo, Kidogo aliowashirikisha P-Square, Make Me Sing alioshirikiana na AKA na zingine, ni nyimbo ambazo kwa Tanzania zinazoonekana hazina utunzi mkubwa, lakini ndizo zinazofanya vizuri nje ya Tanzania na zimetimiza malengo aliyojiwekea.

Anasema kwa kadri jina lake lilivyokuwa likizidi kujulikana Afrika nzima, aliumiza kichwa kuhakikisha anatengeneza muziki ambao watu wa nchi zingine watazielewa na ambao wanahitaji zaidi muziki wa Kiingereza na wa kuchezeka. Amekiri kuwa hiyo ilikuwa ni changamoto kubwa kwake.

“Kule wanataka muziki wa kuchezeka na uwe wa kizungu, nyumbani kwenu hawataki uimbe kizungu, wanataka nyimbo za taratibu, za mapenzi za kuumizwa, kwahiyo uwaridhishe huku na huku. Inabidi uimbe Kiswahili lakini ukishaimba Kiswahili, uweke maneno mafupi ili mtu akremishe,” ameeleza.
“Sometimes hata mashabiki wanalalamika ‘Diamond kuna nyimbo katoa mbona siku hizi uandishi wake mdogo!’ No, mtu haelewi nafocus wapi.”

Diamond amedai kuwa hiyo ndio sababu ameamua kuja na album yake ya Bongo Flava tu.

“Kwanini natoa album yangu ya Bongo Flava? Ni kuonesha kwamba ‘Diamond mnayemsema ninyi ni huyu, ila Diamond huyu anatafuta soko lake na riziki nyingine.’ So ilikuwa tabu kwakuwa kuna muziki mwingine unajua kabisa huu ni wa uongo, lakini huo muziki ndio utakaokufanya uvuke.”

Hitmaker huyo amesema uandishi wa nyimbo kama Ukimwona, Utaipenda, Ntampata Wapi na zingine ni mgumu kufanya vizuri kwenye mataifa mengine ambayo hayaelewi kabisa Kiswahili. Ameeleza ndio maana anaimba nyimbo kama Marry You.

“Kwahiyo lazima ufanye uongo uongo ili wakuelewe, kitu ambacho Tanzania najua hakimake sense lakini ndiyo ukifika ukiimba unachukua kijiji. Kwasababu nikienda kule mimi, ukiimba Ukimwona hawaijui, Kamwambie hawaijui, Mbagala hawaijui, ukiimba hata Ntampata Wapi ambao ni ya mwaka juzi tu hawaijui, Utanipenda hawaijui. Ukiimba Make Me Sing wanaijua, ukiimba Kidogo wanaijua, ukiimba Nasema Nawe wanaijua, Mdogo Mdogo wanaijua sababu ni ya kuamsha, ukiimba Nana wanaijua, Marry You wanaijua sana. Ni nyimbo ambazo nyumbani zimeonekana za kipuuzi. Kweli hata mimi ningekuwa mtu anayetoa ngoma zake ‘huyu naye anapotea dogo’ lakini ndio market ya kule kubwa.”

Diamond amesema ndani ana video ya wimbo wake ambao kila mtu anausifia na alaumu kwanini haitoi, lakini amedai haijatoa sababu ni ya Bongo Flava sana.

“Nitaitoa muda si mrefu sababu kulikuwa kuna kipindi natakiwa niweke mashine za kwenda kote kwasababu sasa hivi nafananishwa na wasanii wakubwa kwenye soko la Kiafrika. Ukifocus utoe nyimbo tu ukimbizane na Mtanzania sababu eti Bongo watazungumza nyimbo yako itahit Tanzania halafu ukivuka tu mpaka haitofika. Kwahiyo wale wa kule wataona Mtanzania kaja halafu kapotea. Kwahiyo ikabidi katikati niachie mashine nyingi za kwenda mbele ili zitengeneze mashow na ili tuheshimiane na watu wa mbele. Kwahiyo kiukweli zimefanikisha na ndio maana sasa naweza kusema natoa nyimbo ya Bongo Flava.”

Mtazame zaidi hapo juu akielezea zaidi suala hili.

Comments

comments

You may also like ...