Header

Taifa Stars kuweka kambi Misri, Mkude kusalia Dar

Kikosi cha wachezaji 20 wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, kinatarajiwa kuondoka kesho Jumanne kuelekea nchini Misri kwaajili ya kambi, kujiandaa na michezo ya kimataifa itakayoanza kutimua vumbi mapema mwezi Juni mwaka huu.
Taifa Stars chini ya Kocha mkuu Salum Mayanga inatarajia kuondoka hapo kesho majira ya saa kumi jioni kwa saa za Afrika ya Mashariki na itaelekea Misri kufanya kambi ya siku nane kujindaa na mchezo wa kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika  dhidi ya Lesotho utakaofanyika Juni 10 mwaka huu katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Wachezaji hao 20 kutoka hapa Tanzania wataungana na wengine watatu wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi ambao ni Nahodha wa kikosi hicho Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu na Faridi Mussa na kufanya jumla ya wachezaji kuwa 23.
Nahodha Msaidizi, Jonas Mkude hataungana na msafara huo kutokana na ushauri wa madaktari walioelekeza kwamba nyota huyo wa Simba hajapata majeraha ingawa anatakiwa apate mapumziko kidogo, hivyo ataungana na kikosi hicho kikirejea jijini Dar es salaam.
Mchezo dhidi ya Lesotho ni muhimu kwa Tanzania ikiwa ni mechi ya kwanza kwa timu hiyo ya Taifa ya Tanzania katika Kundi ‘L’ ya kuwania nafasi muhimu ya kucheza fainali za Kombe la Mataiafa ya Afrika (AFCON) za mwaka 2019 zitakazofanyika nchini Cameroon. Mbali ya Lesotho na Tanzania, mataifa mengine katika Kundi ‘L’ ni pamoja na Uganda na Cape Verde.

Comments

comments

You may also like ...