Header

Mahakama Kuu yaitosa rufaa ya Tigo, yataka iwalipe AY na FA Bilioni 2.1

Mahakama Kuu ya Tanzania imetupilia mbali rufaa iliyofunguliwa na kampuni ya Tigo kupinga kuwalipa wasanii AY na MwanaFA shilingi 2,185,000,000 kwa kutumia nyimbo zao bila kuwalipa.

Wakili Albert Msando ambaye anawakilisha wasanii hao amesema huu ni ushindi muhimu kwa sanaa ya Tanzania. Amenukuliwa akisema, “ni haki yao kulipwa kwa sababu ni kazi zao ambazo zinalindwa kisheria.”

Awali kabla ya rufaa ya Tigo, mwaka jana Mahakama Wilaya ya Ilala, iliamuru kampuni ya MIC Tanzania (Tigo) kuwalipa wasanii hao kiasi hicho cha fedha kutumia nyimbo zao bila idhini.

Tigo walibainika kutumia nyimbo za wasanii hao kwa kipindi tofauti kama miito ya wateja wao na kufanya biashara bila idhini ya wasanii husika.

Hakimu Mkazi Mwanadamizi wa Mahakama ya Ilala, Juma Hassan alitoa hukumu hiyo April 11 mwaka jana, baada ya kuendeshwa kwa kesi hiyo kwa kipindi cha miaka minne. Mbali na shilingi bilioni 2, Tigo waliamriwa kuwalipa wasanii hao shilingi milioni 25 zingine.

Mwana FA aliwaambia waandishi wa habari kuwa uamuzi wa Mahakama ya Ilala ni kitu ambacho kilipaswa kutokea tangu zamani katika tasnia ya muziki ili wasanii wapate haki zao.

“Hiki ni kipindi muhimu kwa Haki Miliki hapa Tanzania,” alisema Mwana FA. Hiki ni kitu ambacho kilikuwa kikifanyika kwa miaka mingi kutokana na kukosekana kwa uelewa na labda gharama za endeshaji wa kesi kama hizo,” alisema Mwana FA.

“Hakuna mtu mwenye haki ya kutumia kazi yako bila ruhusa yako au makubaliano. Na kama amefaidika anapaswa kugawana na wewe kutokana na bei uliyojiwekea kwenye kazi yako,” aliongeza rapa huyo.

Nyimbo ambazo zinadaiwa kutumiwa na Tigo bila idhini ya wasanii hao ni ‘Dakika Moja’ na ‘Usije Mjini’ ambazo zote wamefanya kwa pamoja.

Comments

comments

You may also like ...